SALA YA TOBA

Inawezekana kabisa ya kuwa wewe unayesoma ujumbe huu hujaokoka – yaani hujampokea Yesu Kristo ndani ya moyo wako kama Bwana na Mwokozi wako. Lakini sasa umeona umuhimu wa kumpokea Yesu Kristo katika maisha yako.

Wokovu ni Sasa

Naamini Roho Mtakatifu ameweka fursa hii mikononi mwako kwa mpango maalum wa Mungu ili ufike mahali pa kutubu na kuokoka. Inawezekana kabisa, pia ya kuwa hujawahi kuambiwa juu ya umuhimu wa wewe kuokoka. Lakini napenda kukuambia ya kuwa ni mpango wa Mungu uokoke. Soma Wakolosai 1:13,14 na Yohana 1:12-14 na 1 Timotheo 2:3-6 na Warumi 1:16,17 na Yohana 3:7. Ni vigumu kuona baraka za Damu ya Yesu bila ya kuokoka.

Kwa hiyo kama unataka kuokoka – tafuta mahali palipo na utulivu, na usome kwa sauti sala ifuatayo: (ukiweza unaweza kupiga magoti unapoomba sala hii)

 

Ee Mungu wangu ulie Mtakatifu. Ninakuja mbele zako. Mimi ni mwenye dhambi. Naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha yangu. Ninatubu kweli. Naomba damu ya Yesu Kristo iliyomwagika msalabani kwa ajili yangu initakase sasa katika roho yangu na nafsi yangu na mwili wangu. Nimefungua moyo wangu. Bwana Yesu Kristo nakukaribisha ndani yangu. Ingia kwa uwezo wa Roho wako – uwe Bwana na Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Ahsante kwa kunisamehe na kwa kuniokoa. Nimejitoa kwako nikutumikie katika siku zote za maisha yangu. Shetani hana mamlaka tena juu yangu katika jina la Yesu Kristo. Amina.

Hongera kwa Kuokoka

Ikiwa umesoma sala hii kwa kukusudia kabisa na kwa imani, basi wewe umeokoka na dhambi zako zimesamehewa na kusahauliwa na Mungu sawasawa na alivyoandika katika neno lake. Damu ya Yesu iko juu yako sasa.

Baada ya kuokoka

Unapoanza maisha haya mapya katika Yesu Kristo nakushauri mambo yafuatayo:
1. Zungumza na Mungu kwa maombi kila siku (Yohana 15:7)
2. Soma Neno la Mungu (Biblia) kila siku (Matendo ya Mitume 17:11)
3. Mruhusu Roho Mtakatifu akutawale (Wagalatia 5:16-25; Warumi 8:14-17)
4. Umtumaini Mungu kwa kila jambo katika maisha yako (1Petro 5:7; Zekaria 4:6)
5. Usiache kukusanyika na kushirikiana na wengine waliompokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wao kama wewe ili uimarike zaidi (Waebrania 10:25)

TUNGEPENDA KUSIKIA KUTOKA KWAKO

Karibuuwasiliane nasi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma ya MANA.