Hili ni ombi ambalo, nimemwombea kila mtu anayepata nafasi ya kuusoma ujumbe wangu huu wa Pasaka. Ombi hilo ninalokuombea kwa Mungu ni hili: “Yesu akukumbuke leo katika ufalme wake”.
Ndiyo! Yesu akukumbuke leo, katika ufalme wake! Nimekuombea ombi hili, kwa sababu, “msalaba” ni lango kubwa sana la kiroho. Ni lango la kiroho, ambalo pia linaweza likakufungulia matokeo yake, katika ulimwengu wa kimwili.Kufuatana na Wagalatia 3:13, msalaba uliwekwa kama lango la “laana”. Lakini, tunaona ya kwamba, Yesu alisulubiwa msalabani, ili atubebee adhabu yetu. Adhabu hiyo ilitustahili sisi wanadamu, kwa sababu ya uasi wetu kwa Mungu.Lengo kubwa mojawapo la Yesu kusulubiwa msalabani, lilikuwa ni Mungu kuutumia Msalaba, kama lango la kumpa fursa kila amwaminiye Yesu, apate kupokea Baraka zake kiagano. Hii ni kufuatana na Wagalatia 3:14.
Siku ile Yesu aliposulubiwa, walisulubiwa pia wahalifu wawili – kila mtu katika msalaba wake binafsi. Ukiisoma habari hii katika Luka 23:32, 39 – 43, utaona ya kwamba, mhalifu mmoja aliitumia vizuri fursa ya lango la msalaba. Lakini, mhalifu mwingine, aliitumia vibaya fursa ya lango la msalaba!
Mhalifu aliyeshindwa kutumia vizuri fursa ya lango la msalaba, alijikuta anamsemesha Yesu maneno ya kumkebehi, na kuikebehi fursa ile ya msalaba iliyokuwa mbele yake. Biblia inasema: “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu” (1 Wakorintho 1:18).
Mhalifu aliyeitumia fursa ya lango la msalaba vizuri alimwomba Yesu akisema: “Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako” (Luka 23:42). Na Yesu akampa Mhalifu yule alichoomba (Luka 23:43).
Yesu yuko hai! Na tena, ndiye mfalme wa ufalme wa mbinguni (Wakolosai 1:13, 14).
Ni jambo gani unalotaka Yesu akusaidie, toka kwenye baraka za ufalme wake katika Pasaka hii ya mwaka huu?
Ni maombi yangu kwa Mungu, ya kuwa, utaitumia vizuri fursa ya lango la msalaba mwaka huu, ili kile ambacho Yesu atakupa toka katika ufalme wake, kikupe kumbukumbu nzuri katika maisha yako, tena iwe ya kudumu!
Ndiyo maana, nakuombea katika Pasaka hii, ya kwamba: Yesu akukumbuke leo, katika ufalme wake, kwa kukupa unachomwomba kwenye Pasaka hii!
Mimi na mke wangu, na familia yetu; na Timu nzima ya Huduma ya Mana, tunakutakia Pasaka njema, na yenye baraka!
Usisahau kumshirikisha na mwingine ujumbe huu, ili apokee na maombi yaliyomo ndani yake.
Tuzidi kuombeana. Tunakutakia pasaka njema!