Faida za kuombea akili, ili kuimarisha imani yako, na maisha yako-1

May 5, 2022
Posted in Mafundisho
May 5, 2022 mwakasege

Faida za kuombea akili, ili kuimarisha imani yako, na maisha yako-1

Bwana Yesu asifiwe
Tunaamini unaendelea vizuri. Leo nataka nianze kukuletea mfululizo wa masomo, yanayohusu: “Faida za kuombea akili, ili kuimarisha imani yako, na maisha yako”. Ninapoziandika faida hizi, siziandiki kwa mtiririko wa umuhimu. Naziandika kwa mtiririko wa mfuatano wa kiuandishi tu, faida zote ni muhimu!

Faida ya 1 ya kuombea akili:

MUNGU AKUSAIDIE, KUJUA MATUMIZI YA AKILI ALIZOKUPA, ILI UWEZE KUZITUMIA IPASAVYO, KAMA ALIVYOKUSUDIA.
Mungu alipomuumba mtu, alimuumba awe jumlisho la roho, na nafsi, na mwili (2 Wakorintho 7:1). Mtu ni roho, anayo nafsi, na anakaa ndani ya mwili!
Mtu aliumbwa aweze kuishi, kwenye ulimwengu mbili kwa wakati mmoja – yaani ulimwengu wa kiroho, na ulimwengu wa kimwili kwa pamoja, na kwa wakati mmoja.
Mtu aliumbwa awe roho, ili kwa njia ya roho, aweze kuishi katika ulimwengu wa roho (Mwanzo 1:26, 27). Na kwa mwili wake, aweze kuishi katika ulimwengu wa kimwili (Mwanzo 2:7).
Na mtu alipewa nafsi, ili iwe “kiungo”, kati ya roho na mwili. Na kwa ajili ya jukumu hilo, nafsi ni kiungo muhimu cha mtu, katika kuunganisha maisha yake ya kiroho, na ya kimwili.
Ndiyo maana roho ya mtu, ndiyo iliyoumbwa kwanza (Mwanzo 1:27). Mwili wa mtu, uliumbwa wa pili (Mwanzo 2:7a). Na nafsi ya iliumbwa ya tatu (Mwanzo 2:7b)
Biblia inasema: “Bwana Mungu…, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai” (Mwanzo 2:7). Na ukisoma Ayubu 32:8; utasoma maneno haya: “Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, na pumzi za Mwenyezi huwapa akili”.
Mistari hiyo miwili, inatupa kujua, na kuamini kuwa, akili imo ndani ya Nafsi!
Lakini pia, ni vizuri ujue ya kuwa, akili siyo ubongo, na ubongo siyo akili; ingawa vyote viwili viliumbwa ili vifanye kazi kwa kushirikiana! Ubongo umo katika mwili, na akili imo katika nafsi!
Biblia inatuelekeza tusizitegemee akili! Imeandikwa katika Mithali 3:5, 6; kuwa: “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako”.
Na Mithali 23:4 inasema: “…acha kuzitegemea akili zako mwenyewe”.
Pamoja na maagizo ya biblia, kwamba tusizitegemee akili, inatuhimiza pia, kuwa tuzitumie akili! Hii inatujulisha kuwa, Mungu aliziumba akili ndani ya kila mtu, ili azitumie, lakini asizitegemee!
Biblia inasema: “…Kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya” (Waebrania 5:13, 14).
Faida mojawapo ya kuombea akili, ni ili Mungu akusaidie kujua matumizi ya akili alizokupa, ili uweze kuzitumia hizo akili, kama alivyokusudia!
Tena, kumbuka, bila msaada wa Mungu, si rahisi sana ukaweza kuzitumia akili bila kuzitegemea! Lakini Mungu, anao uwezo wa kukusaidia, uweze kuzitumia akili, na usizitegemee, bali umtegemee Yeye!
Ombea akili ili ujue matumizi yake! Kitu usichojua matumizi yake, ni rahisi kukitumia vibaya; au hutakitumia kwa kiwango kinachotakiwa! Na kitu ulichonacho, na huijui faida yake kwako, si rahisi pia kukikumbuka kukiombea ipasavyo! Zijue faida za akili, ili uweze kukumbuka kuziombea mara kwa mara!
Tuzidi kuombeana katika hili!

TUNGEPENDA KUSIKIA KUTOKA KWAKO

Karibuuwasiliane nasi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma ya MANA.