Bwana Yesu asifiwe.
Heri ya Pasaka ya 2024!
Pamoja na salamu hizo, nataka kukujulisha msaada uliomo ndani ya ufufuo wa Yesu Kristo ili uyashinde majaribu.
Lengo kubwa la majaribu, bila kujali chanzo chake, ni kuijaribu au kuipima “Imani” ya mtu (Yakobo 1:2,3).
Ingawa mazingira yanayoweza kutafsiriwa na mtu ya kuwa ni jaribu kwake ni mengi, lakini vyanzo vikuu vya majaribu ni hivi vifuatavyo:
Chanzo cha kwanza ni Shetani. Biblia inasema: “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi” (Mathayo 4:1). Shetani anapomjaribu mtu, anatengeneza mazingira yatakayotumika kupima imani ya huyo mtu. Shetani anataka katika jaribu hilo, imani ishindwe kumsaidia huyo mtu kuvuka na kulishinda jaribu hilo, ili hatimaye aamue kuiacha imani aliyo nayo kwa Mungu katika Yesu Kristo.
Chanzo cha pili ni Mungu. Biblia inasema: “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu…” (Mwanzo 22:1)
Mungu anapomjaribu mtu, huwa anatengeneza mazingira atakayotumia kupima uwezo wa imani aliyonayo, kama imefikia kiwango cha kuibeba hatua inayofuata ya majukumu na msaada aliompangia huyo mtu.Jaribu kama hili, ni kama mtihani ambao mwanafunzi anapewa kupima uwezo alionao, ikiwa unaweza kubeba masomo ya darasa linalofuata. Ndiyo maana biblia inasema juu ya “toka imani hata imani” (Warumi 1:17). Hii inatupa kujua ya kuwa, kuna ngazi tofauti tofauti za imani, na uwezo wake unatofautiana.
Ndiyo maana mtu anapopokea anachopokea toka kwa Mungu, huwa anapokea kwa kadri ya kiwango cha imani alichonacho!
Chanzo cha tatu ni Tamaa. Biblia inasema: “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe…” (Yakobo 1:14).Neno “tamaa”, kwa jinsi lilivyotumika kwenye mstari huu, lina maana ya msukumo ambao mtu anakuwa nao, unaomsukuma moyoni mwake, ili afanye mambo nje ya mapenzi ya Mungu.
Tamaa inapotumika kama chanzo cha jaribu kwa mtu, lengo lake ni kuipima imani ya mtu, kwa nia ya kuikwamisha ili mtu huyo asitoe ushirikiano kwa Roho Mtakatifu.Ndiyo maana biblia inasema: “Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayoyataka” (Wagalatia 5:16,17).
Na hili lifuatalo unalijua? Ninalotaka ulijue kama hulijui ni kwamba, unapokutana na jaribu kubwa la imani yako, ni kiashiria kinachokujulisha ya kuwa, mbele yako kuna hatua muhimu ambayo Mungu anataka kukupa.
Jaribu toka kwa Shetani, linataka imani yako isikusaidie kulishinda, ili imani hiyo uiache. Na ukiiacha hiyo imani, na kesho yako aliyokupangia Mungu hutaipata (Waebrania 3:16 – 19).
Jaribu toka kwa Mungu, litakujengea msuli wa imani, ili iwe msingi mzuri wa kubebea kesho yako. Soma Yakobo 1:2 – 4
Jaribu toka kwenye Tamaa ya mwili, linatafuta katika mazingira yaliyopo, usiwe na uhakika moyoni mwako juu ya kipi cha kufanya, ili kuifikia kesho yako ambayo Mungu amekupangia (Wagalatia 5:16, 17 na Warumi 8:14).Kwa mfano, Yesu alipokuwa anakaribia kuanza rasmi huduma yake, alikutana na jaribu kubwa toka kwa Shetani (Mathayo 4:1 – 11). Lakini Mungu akamsaidia kushinda! Na mlango ukafunguka wa kuanza huduma yake.
Tena, Yesu alikutana na jaribu kubwa muda mchache kabla ya kusalitiwa na kusulubishwa. Mwili ulikuwa ukishindana na roho yake, juu ya kuyafanya mapenzi ya Mungu ya kunywa kikombe, yaani msalaba (Mathayo 26:36 – 46). Lakini jaribu hili pia, Mungu alimsaidia kulishinda! Na mlango ukafunguka wa Yesu kusulubiwa na kufa na kufufuka!
Yesu alipofufuka ilikuwa ishara mojawapo yenye ujumbe kwa wanadamu ya kwamba, kwa msaada wa nguvu za ufufuo wa Yesu, tunaweza kushinda jaribu lolote linalopima na kuijaribu imani tuliyonayo kwa Mungu katika Yesu Kristo.
Ndiyo maana tunasoma hivi juu ya uhusiano wa ufufuo wa Yesu na imani tuliyonayo kwake: “Tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure” (1 Wakorintho 15:14). “Na kama Kristo hakufufuka, Imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu” (1 Wakorintho 15:17)
Maneno haya “imani yenu ni bure” yana maana ya kuwa imani yetu haina faida, kama Kristo hakufufuka. Hii inatupa kufahamu ya kuwa, kwa kuwa Kristo amefufuka, ina maana imani yetu si bure, bali imani yetu ina faida.Na faida mojawapo tunayoipata katika Yesu aliyesulubiwa na aliyekufa na aliyefufuka, ni imani hiyo kutupa msaada wa kushinda majaribu tunayokutana nayo!
Kwa nini faida ya imani hii imeunganishwa na kufufuka kwa Yesu? Zipo sababu nyingi, lakini leo nikutajie hizi chache, ili zikupe moyo wa kumshukuru Mungu kwa kumfu
fua Yesu kutoka kwa wafu!Sababu ya kwanza:
Yesu Kristo ndiye anadumu kutuombea. Na jambo mojawapo analotuombea, ni ili tupate msaada wa Mungu wa kuyashinda majaribu.
Biblia inasema: “Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea” (Warumi 8:34). Soma pia
Waebrania 7:22 – 25.
Yesu alimwombea Petro, na Petro akashinda jaribu lake. (Luka 22:31, 32). Na Yesu anakuombea na wewe, na utashinda jaribu lako!Sababu ya Pili:
Yesu alipofufuka ilikuwa pia ni ishara ya kutujulisha ya kuwa, malipo ya dhambi zetu aliyoyafanya Yesu pale msalabani, yamekubaliwa na Mungu.
Ndiyo maana imeandikwa ya kuwa: “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu, kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti” (Warumi 8:1, 2).Jambo hili lilifanya shetani na tamaa za mwili, kupoteza uhalali wa kuendelea kutumia dhambi iliyotubiwa, kuishinda imani tuliyonayo katika Kristo Yesu.
Sababu ya tatu:
Nguvu za ufufuo zinaingia ndani yako unapompokea Kristo Yesu moyoni mwako, na kuokoka! Na kwa ajili hiyo, zinamfanya Mungu katika Yesu Kristo, awe pamoja na wewe, ili hata katika majaribu, bado upate nguvu na nia ya kuendelea kuyafanya mapenzi ya Mungu, bila kukata tamaa!
Biblia inasema: “Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa Kondoo, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo” (Waebrania 13:20, 21).Na ndiyo maana nguvu za ufufuo wa Yesu ndani yetu (Waefeso 1:17 – 23), zinatupa kushinda, “na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda” (Warumi 8:37).
Mimi na mke wangu, na watoto wetu, na timu nzima ya huduma yetu ya Mana, tunakutakia siku njema ya kukumbuka kufufuka kwa Yesu.
Tuzidi kuombeana. Tunakutakia pasaka njema!